Author Avatar

bluemouse33

0

Share post:

Wapendwa katika imani,

Marafiki, waumini wenzetu na watu wote wenye mapenzi
mema,


“Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba
yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo”
(1Kor 1:3).

Sisi Makardinali, Maaskofu wakuu na Maaskofu wote wa
Afrika na Madagascar, twawasalimu ninyi wote katika imani na kwa upendo.
Tulipokutana katika Mkutano wetu Mkuu wa 13 wa Maaskofu wa Afrika na
Madagascar” (SECAM), tulijadili mada ya UKIMWI na athari zake mbaya
kijamii. Kwa kufanya hivyo, tumeungana nanyi ndugu zetu waathirika, na
wale wote waliochukua jukumu la kupigana na janga la UKIMWI na athari
zake.

I. TUMESHIKAMANA/ TUMEUNGANA“Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi,
na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja, vivyo
hivyo na Kristo”
. (1Kor 12:12)

Picha hii bora inafafanua vyema mshikamano tunaopaswa
kuuonyesha kwa wale wote wanaoathirika, lakini zaidi kwa kaka na dada
zetu katika Kristo, ambao ni mwili mmoja, pamoja na mamilioni ya
wengineo wanaounda jumuiya ya Wakristu ya Afrika na Madagascar. Ni kwenu
ninyi ndipo tunapouelekeza wito wetu ili tushikamane kulikabili janga
hili ambalo madhara yake hayawezi kuchukuliwa kimzaha na yeyote yule.


Vyema mshikamano huu uambatanishwe na ufahamu wa
madhara ya kuogofya ya janga hili linalotusibu.
Mamilioni ya maisha
yamepotea yakingali machanga, familia zimeteketea au kusambaratika, na
idadi isiyohesabika ya watoto sasa ni yatima na/au ni waathirika. Na
hawa, kuliko wote, ndio wanaohitaji matunzo, malezi, makao, elimu na
watu wazima wa kuwalea.

II. TUWE WAAMINIFU KWA NAFSI ZETU


Sisi kama viongozi wa Jumuiya zetu za Kikristo,
tunajitoa ili kuhakikisha kuwa raslimali ya Kanisa
, iwe vyombo vya
elimu, afya na huduma za kijamaa, vinakuwepo ili kuuhudumia umma.
Tutashirikiana na wafadhili wote ambao wako radhi kusaidia na kufanya
kazi kwa kushirikiana na taasisi za Kikristu na za Kidini. Tuko radhi
kushirikiana nao wote na wale wote walio tayari kutumia vipawa vyao
katika mapambano haya, huku wakifanya hivyo kwa kufahamu kuwa sisi
tunatenda hivyo kufuatia imani yetu katika Injili
. Maana, “mtu
hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha
Mungu
” (Mt. 4:4).

Maadili tuyafundishayo katika jina la Mungu yanalenga
kuheshimu na kuhakiki umuhimu wa uhai wa binadamu, ambao unatunukiwa,
kupata thamani na ubora wake kufuatia ukweli thabiti ya kuwa “uhai ni
zawadi isiyoweza kudhulumiwa au kudhalilishwa itokayo kwa Mungu Baba
anayemwumba kila binadamu na kuwaita wote kwenye utimilifu wa kimaisha”.
Hivyo basi, kujinyima vitendo vya ngono na uaminifu siyo tu njia bora za
kuepukana na maambukizi ya UKIMWI au kuwaambukiza wengine, bali pia ni
njia bora zihakikishazo mwendelezo wa furaha ya kudumu ya kimaisha na
namna ya kufikia utimilifu kamili wa kimaisha.

Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike,
msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana siku zote, kwa kuwa
mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana
” (1 Kor 15:58).

III. TUBADILI MIENENDO


Licha ya kufundisha maadili ya Kikanisa na kuchangia
ueleo wetu wa maadili na jamii nzima, na licha ya kuwaelewesha na
kuwatahadharisha watu juu ya athari za maambukizi ya UKIMWI, tunataka
kuielimisha jamii kiusahihi na kuboresha maadili ya kubadili tabia na
mienendo
tukuzingatia uzuri wa kujinyima vitendo vya ngono,
kujidhibiti kabla ya ndoa na uaminifu katika ndoa. Tunalenga kuuelimisha
umma juu ya “upendo halisi” na elimu ya kijinsia, ili kuwasaidia vijana
na wanandoa wazidi kuvumbua uzuri na ubora wa jinsia zao na baraka ya
uwezo wao wa kuzaa. Kutokana na uzuri na ubora huo uhusiano wa
kujamiiana unapata heshima na kutumiwa kwa namna inayowawajibisha
wahusika, na pia udhibiti wa mpango wa uzazi kati ya mke na mume unakuwa
wa kuheshimiana.


Elimu hii yaweza kuboreshwa na kufanikiwa kama
ushirikiano hai wa walei, wake kwa waume, wote ambao wamekuwa si tu
wakiongelea juu ya taratibu za kimaadili,
bali pia katika ujana wao
na kama wanaondoa, wanatoa ushuhuda hai ya kuwa taratibu na maadili mema
huzaa mahusiano ya kujamiiana yanayoleta uhusiano bora na upendo wa
kibinadamu, na uwajibikaji katika ngono. Elimu hii pia huchangia
katika kuunda familia bora na imara, ambazo kwazo tunapata kinga bora
dhidi ya ukimwi
. Asasi zilizobobea katika utoaji wa elimu ya namna
hii kwa vijana na wanandoa zimetapakaa pote Afrika na zimekuwa zikizaa
matunda ya kutia moyo, licha ya kuwa yaonekana kuwa kidogo. Zote hizi
tunazitia moyo na mhimizo unaozistahili.

IV. TUWAJIBIKE


Mshikamano tuliouongelea hapo awali unatuunganisha na
kutuwajibisha sote katika kukabiliana na changamoto ngumu zenye sura ya
utandawazi: vita sugu na zisizo na vikomo, migogoro na fujo
zinazohusisha ubakaji mara nyingine kama silaha – hii siyo tu kama ni
udhalilisho wa kisaikolojia bali pia ni uangamizaji jamii kwa jinsi
unavyoambukiza na kusambaza UKIMWI.

Tumegundua pia kwamba umaskini huenda sambamba na
UKIMWI.
Inatukereketa sana kuona kuwa uchumi wetu legelege unazidi
kudidimia kufuatia vifo vya wafanyakazi wataalamu na wanataaluma
kutokana na gonjwa la UKIMWI. Umaskini unachangia usambazaji wa virusi
vya UKIMWI, unafanya matibabu na dawa za kinga yawe aghali, unasaidia
kuharakisha vifo kwa waathirika na unazidisha athari za gonjwa hili
kijamii.

Katika haya yote, “Basi kusiwe na faraka katika
mwili, bali viungo vitunzane, kila kiungo na mwenziwe” (1 Kor 12:25).

Mshikamano huu kati yetu na uaminifu wa imani yetu, uamuzi
thabiti wa kubadili mienendo na kuwajibika kwetu kwa ajili
ya umbele wa bara letu, vyote sasa vinapata sura kamili na uelekeo
kufuatia Mikakati ya Kiuetendaji ifuatayo. Tunaiweka mikakati hii mbele
yenu muitumie kwa manufaa yenu.

Mikakati ya Kiutendaji

Sisi Makardinali, Maaskofu wakuu na Maaskofu wa
Afrika na Madagascar, SECAM, tunapendekeza kwa wakleri, mabruda, watawa
wa kike na kiume, waumini na watu wote wenye mapenzi mema, mikakati
ifuatayo ya kiutendaji.2

I. Tukishikamana nanyi, tunaazimia:


 1. Kutumia vyema na kuimarisha vigezo na vipawa vya
  kibinadamu, vya hali na mali/fedha – ambavyo tayari vimetengwa ili
  kukabiliana na janga la UKIMWI katika jumuiya zetu, na kuainisha
  vipengele vya muhimu kiparokia, jimbo na Baraza la Maaskofu mahalia
  ili kusaidia kukusanya takwimu na taarifa muafaka, na mipango ya
  kimaendeleo. Katika hili pia tunaazamia kuunganisha uratibu wa
  jitihada zetu kwenye ngazi ya bara zima ili kupambana na janga la
  UKIMWI.

 2. Kuhakikisha ya kuwa huduma za kiafya za Kanisa,
  huduma za Kijamii na taasisi za elimu zinawajibika ipasavyo kukidhi
  mahitaji ya waathirika wote.

 3. Kuwalenga wanyonge katika jamii, hasa wasichana
  na kinamama wanaobeba mzigo mkubwa kijamii tunapoiangalia hali
  halisi na athari za janga la UKIMWI hapa Afrika.

 4. Kuhamasisha kwa bidii upatikanaji wa matibabu kwa
  wote wasioweza au wanazuiliwa kupata matibabu hayo kufuatia umaskini
  wao na uonevu wa kijamii.

 5. Kuwahusisha kiutafiti wale wote walio waliobobea
  katika dawa asilia/ za kienyeji na kinga asilia ili kufikia ufumbuzi
  na upatikanaji wa njia bora za kujikinga na kupambana na janga la
  UKIMWI.

II. Huku tukiwa waaminifu kwa tunu zetu za Kiinjili,
tunaazimia:

 1. Kushirikiana na Wakristu wa madhehebu mengine na
  dini nyinginezo ambao wanafanya kazi katika jumuiya zao ili
  kuwasaidia waathirika.

 2. Kuhamasisha uhusiano wa karibu zaidi na jamii,
  sekta binafsi/wafanyabiashara, serikali, Umoja wa Mataifa, Jumuiya
  ya Kimataifa, na taasisi za kiserikali na hasa asasi za kuwahudumia
  waathirika, ili kuinua na kuboresha uwezo wake katika kuwatunza na
  kuwahudumia waathirika, bila kupotosha tunu zetu za kiinjili.

III. Tukikabiliana na tishio la UKIMWI,
tunaazimia pamoja nanyi:


 1. Kuhamasisha mabadiliko ya kitabia, mienendo na
  maadili husika katika kupambana na changamoto la UKIMWI.

 2. Kujibidiisha bila kuchoka ili kuondoa dhana
  potofu dhidi ya waathirika na kuwatenga/kuwabagua kijamii, na kuzipa
  changamoto taratibu za kijamii, kidini, kitamaduni na kisiasa na
  mapokeo yote yanayoendeleza hisia potofu zisababishazo kutengwa/kubaguliwa
  kijamii kwa waathirika.

 3. Kuwa msitari wa mbele katika kufutilia mbali
  dhana potofu dhidi ya waathirika na ubaguzi wa kijamii kwa
  kuhamasisha Ushauri na Upimaji Huru (Voluntary Councelling and
  Testing, VCT), ili waathirika waweze kufaidika na matunzo na huduma
  wanazozihitaji. Hii itasaidia pia kuthibiti uambukizaji kati ya mama
  na mtoto.

 4. Kuhamasisha bega kwa bega pamoja na ngazi zote za
  serikali, na asasi zake juu ya utunzi wa miongozo ipasayo kupewa
  kipaumbele na ambayo itasaidia vyema kuwahudumia waathirika,
  kuwaruhusu waathirika kupata huduma na matibabu, kutunza na
  kuuheshimu utu wao katika jamii, na kuyatendea kazi maazimio yote
  yaliyofikiwa katika vikao vya asasi za kiserikali.

IV. Tukiwajibika kwa pamoja, tunaazimia:


 1. Kubuni na kuendeleza mikakati ya kielimu
  inayoshirikisha mada za UKIMWI hasa katika nyanja za tauhidi na
  malezi ya kitawa.

 2. Kuhamasisha na kuimarisha kwa undani zaidi
  tafakari za kitauhidi kuhusiana na tunu za huruma, upendo, uponyaji,
  upatanishi na matumaini, ambazo kwa pamoja zinaweza kupambana na
  vizingiti vya hukumu, aibu na woga – ambavyo mara nyingi huambatana
  na athari za UKIMWI (vikiwalenga waathirika).

 3. Kuandaa warsha kwenye ngazi za kikanda, kitaifa,
  kijimbo na kiparokia ili kuboresha na kukuza upeo, kuleta ufahamu na
  maarifa kuhusu UKIMWI; na kuleta mwamko kuhusiana na masuala ya
  UKIMWI – kuwaelewesha vyema wahusika wote msimamo na maadili ya
  Kanisa kuhusu janga hili.

V. Mwisho, sisi kama wachungaji wa Kanisa –
Familia ya Mungu hapa Afrika kwenye kipindi kigumu cha UKIMWI
,
tunaazimia:


 1. Kuwaanda vvyema kitaaluma wakleri, watawa na
  walei walio na moyo wa kujituma ili waambatane na waathirika katika
  sala na mashauri ya kiroho.

 2. Kutoa malezi kuhusiana na mafundisho ya Kanisa,
  malezi ya kiroho na kijamii – na mafunzo bora katika taaluma za
  elimu dunia, kwa wale wote walio na wito wa kuwahudumia na
  kuambatana na waathirika.

 3. Kuwapokea waathirika makanisani kwa moyo wa
  upendo na huruma, bila kuwahukumu, na “kuwahakikishia nafazi zao
  mezani mwa Bwana.”

 4. Kuwapatia sakramenti na huduma za kikanisa kwa
  taratibu zilizo sahihi na kadri ilivyoombwa na Wakatoliki waathirika.

 5. Kulitendea kazi changamoto lililotolewa na Baba
  Mtakatifu Yohani Paulo II kwa makanisa ya bara letu kupitia Wito
  wake wa Kitume, Apostolic Exhortation, Kanisa Barani Afrika,
  Ecclesia in Africa:

 6. “Vita dhidi ya UKIMWI ni ya kila mmoja wetu.
  Nikirudia wito wa Mababa wa Sinodi, nami natoa wito kwa wahudumu wa
  kichungaji kuleta kwa waathirika, makaka na madada, kadri
  iwezekanavyo tulizo la mahitaji ya kimwili, morali na kiroho. Huku
  nikihimiza, nawaomba viongozi wa nyanja za kisayansi na kisiasa,
  wakisukumwa na pendo na heshima inayomstahili kila binadamu, watumie
  kwa busara njia zote ziwezekanazo ili kusitisha athari za janga hili”.3


Tunadhamiria kuunda kitengo cha huduma kuhusu UKIMWI
kwenye ngazi ya bara zima la Afrika ili kitusaidie kutekeleza Mikakati
yetu ya Kiutekelezaji.

To Love Your HIV+ Neighbour
HOMAGE TO MR. LUBOYA, VICTIM OF HIV/AIDS

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *